MPASUKO WAANZA KUINYEMELEA CCM, MWANZILISHI WA CCJ AYAANIKA MAJINA 37 YA VIONGOZI WA CHAMA HICHO


SIKU moja baada ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutoa tamko la kumtaka aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuacha kukigawa chama kwa madai kuwa hana sifa kuwa rais, mambo mazito yamezidi kuibuka huku ikitolewa orodha ya wanachama wa CCM wakiwemo mawaziri, wabunge na makada maarufu wanaodaiwa kukisaliti chama hicho.
 
Hatua hiyo imeenda sambamba na kumtaka Katibu wa Umoja wa Vijana Uhamasishaji na Chipukizi, Paul Makonda, kuacha kuwanyooshea vidole wenzao, wakati ndani ya chama hicho kuna wasaliti wakubwa na wasiokuwa na usafi wowote wa kuwasema wenzao.
 
Hayo yamewekwa hadharani Dar es Salaam jana na aliyekuwa Mwenyekiti na mwanzilishi wa CCJ Taifa, Richard Kiyabo, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano Idara ya Habari (MAELEZO).
 
Kiyabo aliitaka CCM kusafisha wanachama wasio waaminifu ambao ni mamluki wakiwemo mawaziri, wabunge machachari na makada maarufu kutokana na kushiriki kwao kuanzisha Chama Cha Kijamii (CCJ) huku bado hawajarejesha kadi za chama hicho.
 
Kiyabo alisambaza kwa waandishi wa habari orodha ya wanachama wa CCM 37 anaodai walishiriki kutoa michango ya fedha kwa ajili ya kufanikisha maandamano ya amani ya CCJ yaliyolenga kupinga uonevu wa msajili wa vyama vya siasa nchini.
 
Alisema tayari ameshamwandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula kukiomba chama kichukue hatua za kinidhamu na kimaadili kwa wanachama ambao si waaminifu na tayari walikwishapoteza sifa za kuwa wanachama, kutokana na kushirikiana nao kuanzisha CCJ, huku wakiwa wanachama  wa CCM.
 
"Kitendo cha kuwa wanachama wa vyama viwili kwa wakati mmoja ni kosa kubwa na ni usaliti ndani ya chama, kosa hili halipishani na kosa la uhaini ndani ya chama, lakini kwa masikitiko yangu makubwa watu hawa hadi sasa hawajaitwa na vikao vya chama wala hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa au kujadiliwa kwa makosa ya kukisaliti chama na kuamua kuwa mamluki ndani ya chama," alisema Kiyabo.
 
Alisema mwanzoni mwa mwaka 2010 walipokubaliana kuanzisha CCJ malengo makuu ilikuwa chama hicho kushiriki uchaguzi mkuu na kusimamisha mgombea wa kiti cha urais na wabunge, pamoja na madiwani kama wangekidhi matakwa ya kisheria.
 
"Nashangaa ndani ya CCM bado kuna wanachama na viongozi waandamizi wana kadi mbili za CCJ na CCM na wanashindwa kuzirudisha na hata kukana, ikiwemo kuwaomba radhi wanachama kwa kitendo cha usaliti," alisema na kuongeza kuwa anawashangaa baadhi ya wanachama ambao si waaminifu ndani ya chama.

Mbele ya waandishi wa habari, Kiabo aliwataja waasisi hao wa CCJ na fedha walizochangia  kwenye mabano kuwa ni pamoja na  Dk. Harrison Mwakyembe (sh 300,000), Samuel Sitta (sh 500,000), Anne Kilango (sh 400,000), Nape Nnauye (sh 100,000), Paul Makonda (sh 100,000) na James Lembel (sh 400,000) ambao kwa sasa ni miongoni mwa wanachama wa CCM wanaotajwa kuwa na makundi ya urais.
 
Wengine ni Amina Katemi (sh 300,000), Alex Kisumo (sh 300,000), Baraka Seif (sh 300,000), Sospeter Banigwa (sh 300,000), Saleh Omari (sh 300,000), Sarah Patrick (sh 200,000), Daniel Mwaijojeli (sh 200,000), Dk. Ngonyani (sh 300,000), Elisha Eliya (sh 200,000), Emanuel Magonja (sh 200,000) na Asma Watosha (sh 300,000).
 
Pia wamo, Kulwa Lulelema (sh 50,000), Hamadi Maduku (sh 100,000), Flavian Nkya (sh 100,000), Gulam kutoka Zanzibar (sh 150,000),  Hamad Ferej (sh 200,000), Ally Harun (sh 50,000), Masudi Kangi (sh 100,000), Gumbo (sh 150,000), Idd Kiriwe (sh 100,000), Innocent Makala (sh 200,000), Jacob Msambya (sh 200,000),  Ishelula (sh 150,000), Kipute (sh 200,000), Joseph Kashindye (sh 200,000) Kamala Ng’ombe (sh 200,000) na Daniel Malongo (sh 50,000).
 
Alisema ni vyema wakati huu kuelekea uchaguzi CCM ianze kujisafisha ili wale mamluki waumbuke na wasipewe nafasi ya kugombea wakati ukifika
 
Makonda alipoulizwa kuhusiana na madai hayo alijibu kuwa anaelewa kuwa mchezo huo unachezwa na vibaraka kwani suala hilo halina uzito ndani ya chama.
 
Alidai kuwa suala la kuondoa watu wanaotumiwa na Lowassa kukihujumu chama hicho halijibiwi. Alisema ni muhimu kuelewa kuwa wapambe wote wa Lowassa watatoka na watakapomalizika atashughulikiwa yeye kichama kwani ndiye tatizo.
 
“Wapambe wote watoke na watakapoisha tutashughulika na bosi wao anayewatuma... ninajua hawajajipanga ndiyo maana wamekurupuka na kuja na hoja rahisi," alisema.
 
Alisema wanamtaka Lowassa akanushe kuwatumia hao watu. Kwa Nape, alisema yalishajadiliwa na mjadala kufungwa ndani ya chama, hivyo madai hayo si mapya hawezi kuyazungumzia.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

Post a Comment

Ungana Nasi, Like Page Yetu Hapa Chini