MAMA mmoja mkazi wa
Ronsoti, Kata ya Nyamisangura, wilayani hapa, Eliza Marwa,28, hivi
karibuni amenusurika kuuawa na mumewe, baada ya majirani kufika kumuokoa
kutokana na kukatwakatwa mapanga.
Mariamu akiugulia maumivu.
Mama huyo aliliambia gazeti hili akiwa katika Hospitali ya Wilaya
Bomani, Tarime kuwa mume wake Marwa Ogora alimkatakata mapanga baada ya
kumtuhumu kuwa akikwenda kwa hawara yake badala ya kwenda kwenye mazishi
ya mjomba wake huko Bunchari.
“Nilichukua jukumu la kwenda kwa kutumia nauli yangu kwa kuwa muda
huo mume wangu alikuwa kazini na baada ya mazishi kesho yake asubuhi
Desemba kumi na saba mwaka huu nilirudi nyumbani na kumkuta mume wangu
ambaye alianza kunipiga kwa mpini wa jembe kisha panga akidai kuwa
sikuwa nimeenda kwenye mazishi badala yake nilikuwa nimeenda kwa mpenzi
wangu.
“Alinishambulia sehemu mbalimbali za mwili hususani kichwani, kidogo
anitoe ubongo, wasingekuwa majirani kuniokoa baada ya kupiga yowe
naamini angeniua kwani hivi sasa siwezi hata kuamka na masikio yameziba,
miguu ina ganzi, siwezi kutembea.
“Mume wangu Ogora amekuwa akinipiga mara kwa mara lakini kutokana na
watoto tuliozaa naye nimekuwa nikivumilia mateso, naogopa kuondoka na
kuacha watoto walelewa na mama wa kambo,”alidai mama huyo.
Ogora hakupatikana kuzungumzia tukio hilo kwani anasakwa na dola na
afisa mmoja wa polisi wilayani hapa wamethibitisha kutokea kwa tukio
hilo na akasema wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa. Naye daktari wa
hospitali aliyolazwa mama huyo, Nega Malico alikiri kumpokea mgonjwa
huyo.
0 comments:
Post a Comment