Itakumbukwa kwamba tarehe 19 Februari 2014 Mwenyekiti wa Muda wa Bunge
Maalum Pandu Kificho aliteua Kamati ya Wajumbe ishirini yenye uwakilishi
wa makundi yote yanayounda Bunge Maalum kwa ajili ya kumshauri kuhusu
Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum.
Rasimu ya kwanza ya Bunge Maalum iliandaliwa na Kamati ya Maandalizi
chini ya Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar (
nakala yake niliwapa hapa).
Kazi ya mjumbe ni kuwakilisha na kuwasilisha; katika kutekeleza wajibu
huo, jana 26 Februari 2014 tulikuwa na Semina ya Bunge Maalum kuhusu
Rasimu ya Pili ya Kanuni za Bunge Maalum toleo la 2014.
Katika mjadala wa jana niliunga mkono mapendekezo ya rasimu katika
sehemu ya nne kuhusu kupunguzwa kwa mamlaka na madaraka makubwa ya
Mwenyekiti wa Bunge Maalum, tofauti na rasimu ya kwanza; sasa maamuzi ya mwenyekiti hayatakuwa ya mwisho.
Mjumbe
asiporidhika anaweza kukata rufaa na pia rasimu sasa inapendekeza kwamba
mwenyekiti au makamu wanaweza kuondolewa kwa kura ya kutokuwa na imani.
Niliunga mkono kuruhusiwa kwa utaratibu wa kuwasilisha Taarifa ya Maoni
Kinzani (dissenting opionion); hii ni kwa sababu rasimu ya kwanza
haikuwa na utaratibu wa uwasilishaji bungeni wa hoja za wabunge, hoja
zote ilikuwa ni kamati.
Njia pekee ya kuwezesha mawazo mbadala kuweza
kufika katika ukumbi wa Bunge kwa ukamilifu ukiondoa michango ya wabunge
ni kupitia Taarifa za Maoni Kinzani.
Utaratibu huu utawezesha pia kufanya wajumbe walio wengi wenye msimamo
unaofafanana kuepusha uwepo wa maoni kinzani kwa kujadiliana na
kuridhiana na wachache wenye maoni ya msingi bila kujali idadi yao na
hivyo kujenga muafaka wa kitaifa.
Taarifa ya Maoni Kinzani isiporuhusiwa
upigaji kura utatumika kwa haraka kupitisha msimamo wa wengi bila
kutafakari kwa kina mtizamo wa wachache ndani ya kamati ambao wakati
mwingine unaweza kuwa unawasilisha maoni ya wananchi wengi nje ya Bunge.
Nimeunga mkono utaratibu wa kura ya siri kutumika kupitisha hoja za
kamati na masharti ya Rasimu ya Katiba ibara kwa ibara na hatimaye
kupitisha rasimu ya mwisho ya katiba. Mtizamo wangu wa awali ulikuwa ni
kura kuwa ya wazi kwa kuzingatia kwamba wajumbe ni wawakilishi.
Hivyo,
ni muhimu wanaowawakilisha wakafahamu wawakilishi wao wamesimamia upande
gani na pia kuwezesha kila mjumbe kuwajibika kutokana na kura yake.
Aidha, kura ya wazi inaweza kudhibiti wajumbe dhidi ya ushawishi usio
sawa (undue influence) ikiwemo unaowezesha kuhusisha ufisadi kwa kuwa
mjumbe atajulikana wazi iwapo atakwenda kinyume cha maoni ya wananchi
kwenye masuala ya msingi kwa sababu ya ushawishi huo.
Kwa kuzingatia mtizamo huo, nilipendekeza kwa wenzangu kwamba kura ziwe
za mchanyato/mchanganyiko; katika hatua ya kwanza ya kura kupigwa wakati
wa kupitisha ibara moja moja ya katiba, kura ya siri itumike. Ili
wajumbe wawe huru katika hatua hiyo kupigia kura ibara kwa ibara kwa
kadiri ya ripoti za kamati na majadiliano.
Lakini kura ya mwisho, baada
ya kuwa ibara zote zimekubaliwa; ya kupitisha katiba kwa ujumla wake
basi kura iwe ni ya wazi ya kuitwa jina mjumbe mmoja mmoja kama ambavyo
Bunge hufanya wakati wa kupitisha bajeti.
Hata hivyo, baada ya kupata Waraka na. 3 wa Siri wa CCM kuhusu Rasimu ya
Katiba wa Februari 2014 ambapo pamoja na mambo mengine ni wa ‘kujipanga
vizuri katika hatua zinazofuata za mchakato wa kuunda katiba mpya’
ikiwemo katika Bunge Maalum na kusikiliza michango ya baadhi ya wajumbe
jana niliona wazi kwamba watetezi wa kura ya siri wana ajenda ya siri
nyuma yao.
Katika mazingira hayo, ili kuwezesha uhuru wa wajumbe katika uamuzi kwa
kuzingatia maoni ya wananchi na majadiliano yatayofanyika bungeni kwa
lengo la kujenga muafaka wa kitaifa katika mchakato wa katiba nimeamua
kwa nia njema kuwa mtetezi wa kura ya siri kutumika katika Bunge Maalum.
Kila mjumbe awezeshwe kuwajibika kwa nchi yake, nafsi yake na Mungu wake
kwa kuzingatia maoni ya nchi na maslahi ya taifa badala ya kupiga kura
kwa kuhofia msimamo wa chama, taasisi au kundi analoliwakilisha katika
Bunge Maalum.
Nilieleza wazi kwamba wanaopendekeza kuwa ibara za rasimu ya katiba
zipitishwe kwa wingi wa kawaida (simple majority) na kwamba wingi wa
theluthi mbili utumike wakati wa kuamua kuhusu rasimu ya mwisho pekee
wanataka Bunge Maalum lipitishe kanuni inayokwenda kinyume na Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ambayo kimsingi itakuwa batili.
Nilieleza kwamba watetezi wa hoja hii wanasoma sheria toleo la Kiswahili
pekee ambalo lina makosa; kifungu cha 26 (2) kinasema “Ili katiba
inayopendekezwa iweze kupitishwa” wakati ambapo ya Kiingereza inasema
“The provisions of the proposed constitution shall require passing by”;
kwa maana ya kwamba inazungumzia vifungu.
Aidha, pamoja na kuwa Sheria
hiyo hiyo toleo la Kiswahili 32 (4) inasema matoleo ya Kiingereza na
Kiswahili “yote ni sahihi” , toleo la Kiingereza limesema “are
authentic”; kwa maana ya kuwa ni halisi.
Mgongano huo baina ya sheria mbili unapatiwa ufumbuzi kwa kurejea sheria
zingine na maamuzi ya mahakama ambapo inaonyesha kwamba kunapotokea
mgogoro baina ya matoleo ya lugha zingine za sheria ile ya Kiingereza
inatamalaki. Hivyo, kwa kuwa sheria hizo zinazotukuza Kiingereza bado
hazijabadilishwa, sheria inayopaswa kuongoza Kanuni ni ya Kiingereza
ambayo imeweka bayana kwamba vifungu vitapitishwa kwa kura ya wingi wa
mbili ya tatu.
Napendekeza kwamba masuala haya manne ambayo kuna mwelekeo kwamba kuna
watu wamekutana juzi, kabla ya mjadala wa jana kupanga kwamba maoni ya
kamati yasikubaliwe yanapaswa kuungwa mkono na wajumbe na wananchi nje
ya Bunge.
Pamoja na kuunga mkono masuala hayo, yapo marekebisho ambayo
nimependekeza kwa maandishi yafanyike na mengine nitaendelea
kuyapendekeza leo na kesho.
Katika muktadha huo, naiweka hapa nakala ya
Rasimu ya Pili ya Kanuni za Bunge Maalum ili nawe ushiriki kutoa maoni
na kushawishi wajumbe unaoweza kuwafikia ili kwa pamoja tuhakikishe
zinatungwa bora zitazowezesha Bunge Maalum kuendeshwa kwa ufanisi katika
kuiboresha rasimu na kuifanyia mabadiliko mazuri kwa kuzingatia maoni
ya wananchi na maslahi ya nchi.
Wenu katika uwakilishi wa umma,
John Mnyika (Mb)
27/02/2014
Dodoma